Shilingi Bilioni 5.5 zazuiliwa na serikali

0
773

Serikali imezuia Shilingi Bilioni 5.5 ambazo zilipaswa kutumika kutekeleza mradi wa kimkakati wa Soko la Magomeni lililopo wilayani Kinondoni mkoani Dar es salaam kutokana na kucheleweshwa kwa utekelezaji wa mradi huo.

Uamuzi huo umetangazwa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Ashatu Kijaji baada ya kutembelea na kukagua ujenzi wa mradi huo unaotarajia kugharimu Shilingi Bilioni Tisa, na kukuta ujenzi wake hauridhishi.

Dkt Kijaji amesema kuwa serikali imeipatia Manispaa ya Kinondoni Shilingi Bilioni 3.5 tangu mwezi Mei mwaka 2018 kwa ajili ya kutekeleza mradi huo ambao ungepaswa ukamilike ndani ya miezi Tisa tangu kusainiwa kwa mkataba wake, lakini ameshangaa kutomkuta Mkandarasi kwenye eneo la ujenzi.

Awali akitoa maelezo ya mradi huo wa kimkakati wa Soko la Magomeni, Mhandisi wa Manispaa ya Kinondoni,- Justin Lukaza ameeleza kuwa Manispaa hiyo imeingia mkataba wa kujenga soko hilo litakalokuwa na ghorofa tatu na kwamba ujenzi wa mradi huo ungekamilika katika kipindi cha miezi Sita ijayo.

Hata hivyo maelezo hayo yalitofautiana na yale ya Mkandarasi ambaye alimweleza Dkt Kijaji kuwa ujenzi huo utachukua muda wa miezi 12.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni,-Daniel Chongolo amekiri kuwa kuna uzembe umefanywa na watendaji wa Manispaa ya Kinondoni uliosababisha mradi huo kuchelewa kuanza.

Chongolo amemuomba Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Ashatu Kijaji ampe muda mfupi wa kurekebisha kasoro hizo.

Amesema kuwa tayari kuna hatua mbalimbali zilichukuliwa kwa maafisa waliofanya uzembe katika utekelezaji wa mradi hapo awali na hakujua kama bado kulikuwa na uzembe uliokuwa unaendelea baada ya kuchukua hatua hizo kwa sababu aliamini watendaji waliokabidhiwa kusimamia ujenzi wa mradi huo walijifunza kutokana na makosa ya wenzao walioondolewa kusimamia mradi huo.

Mradi wa Soko la Kisasa la Magomeni ni miongoni mwa miradi 22 iliyopewa ruzuku na Serikali katika Mpango wa Awamu ya Kwanza wa kuziwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa kujitegemea kimapato, ambapo zaidi ya Shilingi Bilioni 147 zilitolewa na Wizara ya Fedha na Mipango kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo.