Rais Samia kufungua mkutano wa Shirika la Utalii Duniani

0
351

Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa mkutano wa 65 wa Shirika la Utalii Duniani Kamisheni ya Afrika, utakaoanza tarehe 5 Oktoba 2022 jijini Arusha.

Lengo la mkutano huo ni kujadili mustakabali wa ustawi wa maendeleo ya sekta ya utalii barani Afrika, hasa baada ya athari za mlipuko wa janga la UVIKO -19 lililoathiri utalii wa kimataifa kwa wastani wa kati ya asilimia 50 na 85 katika nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania.

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Pindi Chana amesema kuwa, mkutano huo ni muhimu kwa kuwa ni mojawapo ya jitihada za Serikali katika kuongeza idadi ya watalii na kutanua wigo wa mazao ya utalii nchini kupitia uendelezaji wa mazao ya utalii ya kimkakati hususan utalii wa mikutano na matukio.

Amesema kuwa mkutano huo pia utawezesha kujengea uwezo wataalam na wadau wa utalii katika kutangaza utalii, kuendeleza na kufungamanisha mazao ya utalii katika kanda mbalimbali za utalii nchini kulingana na shabaha ya kuongeza idadi ya watalii kufikia milioni 5 na mapato ya dola bilioni 6 za Kimarekani ifikapo mwaka 2025.

Kauli mbiu ya mkutano ni ‘Kuujenga Upya Utalii Stahimilivu wa Afrika kwa Maendeleo Jumuishi ya Kiuchumi na Kijamii.”