Majaliwa: Utoaji elimu bora ni kipaumbele cha nchi

0
159

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa sekta ya elimu ni wakala muhimu wa mabadiliko katika jamii kiuchumi, kiteknolojia na kiutamaduni, mambo ambayo yanachochea maendeleo ya nchi na hivyo utoaji wa elimu bora kwa Watanzania ni moja ya vipaumbele vya nchi.

“Ili kufanikisha haya tunahitaji sekta hii kuwa bora, imara, inayokidhi mahitaji ya jamii kwa kuwapa vijana maarifa na ujuzi wa kukabiliana na matatizo ya kijamii, kitaifa na kimataifa,” amesema.

Amesema hayo leo Machi 25, 2024 wakati wa mkutano wa wadau wa Sekta ya Elimu mkoani Dodoma uliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Biblia-TAG.

Majaliwa amesema Rais Samia Suluhu Hassan ni mdau namba moja wa sekta ya elimu na ndio maana katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake amewekeza katika kuweka mazingira bora ya utoaji elimu na kuhakikisha Serikali inaendelea kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo katika sekta ya elimu.

“Ninaamini sisi sote ni mashuhuda wa jinsi Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kipindi cha uongozi wake alivyotekeleza kwa vitendo azma ya kuhakikisha elimu bora inapatikana kwa watoto wote wa Kitanzania bila kujali jinsia wala hali ya kiuchumi,” amesema.

Ametaja baadhi ya maeneo ambayo Rais Samia ameyasimamia kikamilifu kuwa ni mpango wa uboreshaji wa miundombinu ya elimu, ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi, mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na mapitio ya sera ya elimu na mafunzo.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amewataka viongozi katika halmashauri nchini kuhakikisha fedha zinazoletwa kwa ajili ya kulipa stahiki mbalimbali za walimu hazipangiwi matumizi mengine.

“Walimu wapewe stahiki zao mara moja ili kuondoa malimbikizo ya madeni yasiyo ya lazima na manung’uniko dhidi ya Serikali bila sababu,” amesema.

Kwa Upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia shilingi bilion 92.4 zimetolewa kwa ajili miundombinu ya elimu mkoani humo.