Kimbunga HIDAYA kinasogea Pwani ya Tanzania

0
95

Kimbunga “HIDAYA” kimeendelea kuimarika na kusogea kuelekea maeneo ya pwani ya Tanzania ambapo hadi kufika saa 9 usiku wa tarehe 03 Mei 2024 kilikuwa kimeimarika zaidi na kufikia hadhi ya Kimbunga kamili kikiwa umbali wa takribani kilomita 401 Mashariki mwa pwani ya Mtwara.

Taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema “katika kipindi hiki kimbunga HIDAYA kimeendelea kuimarika zaidi huku kasi ya upepo ikiongezeka hadi kufikia kilomita 130 kwa saa.”

Taarifa hiyo imeeleza kuwa Mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa baharini bado inaonesha uwezekano mkubwa wa Kimbunga HIDAYA kusalia katika hadhi ya Kimbunga kamili kwa saa 12 zijazo huku kikiimarika, na kendelea kusogea karibu kabisa na pwani ya Tanzania.

TMA imeeleza kuwa Kimbunga hicho kinatarajiwa kuendelea kuwepo hadi tarehe 06 Mei 2024 na kupungua nguvu baada ya hapo.

Taarifa hiyo imesema “uwepo wa Kimbunga HIDAYA karibu na pwani ya nchi yetu unatarajiwa kutawala na kuathiri mifumo ya hali ya hewa hapa nchini ikiwa ni pamoja na kusababisha vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, visiwa vya Unguja na Pemba na maeneo ya jirani.”

Mamlaka ya Hali ya Hewa imewashauri wananchi katika maeneo ya pwani na wanaojihusisha na shughuli mbalimbali baharini kuchukua tahadhari kubwa na pia kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri na tahadhari pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kujikinga na athari zinazoweza kujitokeza.