FMO yashusha neema kwa wanawake na vijana

0
223

Benki ya Maendeleo ya Wajasiriamali ya Uholanzi (FMO)
imetoa mkopo wa dola milioni 125 za kimarekani ambazo ni sawa na shilingi bilioni 292.5 kwa benki ya NMB, lengo likiwa ni kuwanufaisha wanawake na makundi yanayojihusisha na kilimo – biashara.

FMO pia imesaini mkataba wa mradi wa NASIRA na benki ya NMB, wenye thamani ya dola milioni 11 za kimarekani kwa ajili ya kufadhili biashara ndogo na za kati nchini.

Mradi wa NASIRA umelenga kuyanufaisha maeneo ambayo yanaonekana kutopewa kipaumbele yakitajwa kuwa ni yale ya biashara zinazomilikiwa na wanawake na vijana.

Mradi huo wa NASIRA unafadhiliwa na Umoja wa Ulaya na Serikali ya Uholanzi, ambapo hadi sasa mikataba 11 imekwishasainiwa kwenye nchi za Afrika yenye thamani ya dola milioni 270 za kimarekani.

Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ndio kitovu cha mradi huo na hadi sasa zimepatiwa dola milioni 80 za kimarekani.

Mikataba hiyo miwili imesainiwa leo mkoani Dar es Salaam na kushuhudiwa na Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi ikiwa ni siku ya pili na ya mwisho ya Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya.