Changamoto ya barabara Geita yapata jawabu

0
259

Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANRODS) imekusudia kutekeleza miradi saba ya kimkakati ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami mkoani Geita, baada ya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kukamilika.

Meneja wa TANROADS mkoani Geita, Ezra Daniel ametaja miradi ambayo Serikali imekusudia kuijenga kuwa ni pamoja na barabara ya Geita – Nzera – Nyamadoke (km 50), Mtakuja – Buhalahala (Geita mjini) km 24 na Nyankumbu – Nyang’wale/Busolwa – Kharumwa – Nyang’holong hadi kahama (km 162), ambapo kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024 tayari Serikali imetenga fedha ili barabara hizo zitangazwe na kumpata mkandarasi ambaye ataanza kazi ya ujenzi.

Amesema lengo la Serikali ni kujenga barabara kwenye kila wilaya Mkoani Geita ikiwemo kufanya stadi ya kuweza kuijenga barabara ya njia nne Geita Mjini ili kurahisisha usafirishaji wa Wafanyabiashara wa madini kutoka Geita kwenda kuuza nchi jirani kupitia miundombinu ya barabara.

Naye Mkurugenzi wa matengenezo kutoka TANROADS Mkoa wa Geita Mhandisi Fredrick Mande ameishukuru Serikali ambayo katika kipindi cha miaka mitatu imeendelea kutoa fedha ambazo zimetumika na zinaendelea kutumika kwa ajili ya kazi ya matengenezo ili kunusuru barabara zisijifunge.