Barrick Gold kutekeleza makubaliano yake na Tanzania

0
670

Rais John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Afisa Mwendeshaji Mkuu wa Kampuni ya Barrick Gold anayeshughulikia Afrika na Mashariki ya Kati Dkt Willem Jacobs Ikulu jijini Dar es salaam.

Baada ya mazungumzo hayo Dkt Willem amesema wamekutana na Rais Magufuli ili kumhakikishia kuwa makubaliano yaliyofikiwa Oktoba 19 mwaka 2017watayatekeleza kikamilifu hasa baada ya kampuni kubwa ya uchimbaji dhahabu ya Rand Gold ya Afrika Kusini kuungana na Barrick Gold Corporation katika Umiliki, Uwekezaji na Menejimenti.

Dkt Willem amebainisha kuwa hakuna kitakachokuwa tofauti na makubaliano yaliyofikiwa awali ambayo yaliongozwa na Mwenyekiti Mtendaji wa Barrick Gold Corporation Profesa  John Thornton ikiwemo kampuni hiyo kuilipa Tanzania kifuta machozi cha Dola Milioni 300 za Kimarekani ambazo ni sawa na Shilingi Bilioni 682.5, kuendelea na uwekezeji kwa ubia kati ya Tanzania na Kampuni ya Barrick Gold na mgawanyo wa mapato ya kiuchumi kwa uwiano wa asilimia 50 kwa 50 kati ya Tanzania na kampuni ya Barrick Gold.

Amempongeza Rais Magufuli kwa jitihada zake za kusimamia rasilimali za nchi na kwamba anaunga mkono jitihada  hizo kwa kuwa ndio mwelekeo sahihi ambao nchi za Afrika zinapaswa kuufuata.

“Mimi ni Mwafrika na sisi sote ni Waafrika, anachokifanya Rais Magufuli ni sahihi kabisa, anahakikisha utajiri wa rasilimali uliopo unabainishwa na unawanufaisha Watanzania, ndio maana tupo hapa kwa sababu tunakubaliana naye, na hivi ndivyo sisi Waafrika tunapaswa kufanya kwa rasilimali zetu”,  amesema Dkt Willem.

Kwa mujibu wa Afisa Mwendeshaji Mkuu wa Kampuni hiyo ya Barrick Gold anayeshughulikia Afrika na Mashariki ya Kati Dkt Willem, baada ya muungano huo wa Rand Gold na Barrick Gold Kampuni mpya ya Barrick Gold imekuwa kampuni kubwa inayoongoza kwa umiliki wa rasilimali za dhahabu duniani ikimiliki rasilimali Tano  kati ya Kumi.

Amesisitiza kuwa kutokana na uwezo huo, Barrick Gold Corporation  sasa imeweza kujiimarisha zaidi kiuwekezaji na utaalamu na ipo tayari kushirikiana na Tanzania ili kuhakikisha rasilimali ya dhahabu iliyopo inaleta manufaa kwa pande zote mbili yaani Watanzania na mwekezaji.

Kwa upande wake Waziri wa Katiba na Sheria Profesa  Palamagamba Kabudi ambaye ameongoza timu ya majadiliano kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Barrick Gold amesema kuwa nyaraka za makubaliano hayo zimekamilika na kwamba sasa kinachosubiriwa ni utekelezaji wa makubaliano hayo unaotarajiwa kukamilika ifikapo mwisho wa mwezi Machi mwaka huu.

 “Baada ya muungano wao yani Rand Gold na Barrick Gold Corporation, hii sasa ni timu mpya na tumewaona ni watu ambao sasa wapo tayari kutekeleza yale yote yaliyokubaliwa, na sasa ni kwa kila upande kwenda kwenye vyombo vyake vinavyohusika kufanya maamuzi ya mwisho ili utekelezaji ufanyike” amesema Profesa Kabudi.