Wayakumbuka mateso ya Yesu kwa kupigiliwa msalabani

0
256

Ikiwa leo ni siku ya Ijumaa Kuu kwa Waumini wa dini ya Kikristo, wengi huitumia siku hii kufanya Ibada na kuyakumbuka mateso ya Yesu Kristo.

Wengine wamekuwa wakiigiza na wengine wakifanya uhalisia wa mateso yanayoelezwa kuwa aliyapitia Yesu Kristo.

Baadhi ya Waumini wa dini ya Kikristo wa madhehebu ya Kikatoliki wameonekana wakiwa wametundikwa kwenye misalaba ya mbao huku wengine wakipigwa mijeledi migongoni na kuchuruzika damu ikiwa ni maigizo katika Ibada ya Ijumaa Kuu.

Ingawa watu wengi katika nchi zenye Wakatoliki wengi hutumia siku ya Ijumaa Kuu kwenye Ibada au kutulia majumbani pamoja na familia zao, wengine hujitahidi kupitia mateso kiasi kama sehemu ya kulipia dhambi zao au kukumbusha desturi zinazoonekana kupuuzwa.

Huko nchini Ufilipino katika kijiji cha San Juan, Kaskazini mwa Manila, mamia ya wakazi na watalii wameshuhudia uigizaji wa mateso yanayoelezwa kuwa aliyapitia Yesu Kristo wakati anakaribia kutimiza safari yake ya mwisho duniani.

Makumi ya Wanaume waliovalia taji zilizotengenezwa kwa mizabibu na kitambaa usoni wameonekana wakitembea bila viatu kwenye mitaa mbalimbali, huku wakipigwa kwa mijeledi ya mianzi migongoni mwao.

Katika hatua ya mwisho ya onesho hilo, Wanaume watatu ambapo wawili kati yao walikuwa wamefungwa kwenye misalaba ya mbao walisindikizwa na maakida wa Kirumi hadi kwenye kilima ambapo ndipo walipotundikwa msalabani.

Wilfredo Salvador, ambaye anajishughulisha na uvuvi nchini humo aliigiza nafasi ya Yesu Kristo, ambapo alipigiliwa misumari kwenye viganja vya mikono yake na miguu yake huku ndege zisizo na rubani (drone) zikirushwa juu na watalii kupiga picha na kuchukua video kwa simu zao.

Baada ya dakika kadhaa, misumari hiyo ikang’olewa na Salvador akashushwa chini na kupokelewa kwa machela hadi kwenye hema la matibabu kwa ajili ya uchunguzi.