Sasa rasmi watafuta hifadhi Uingereza kupelekwa Rwanda

0
119

Muswada wa Waziri Mkuu wa Uingereza, Rishi Sunak wa kuwapeleka wahamiaji Rwanda unatarajiwa kuwa sheria baada ya miezi mitano ya mabishano baina ya ofisi ya Waziri Mkuu huyo na Bunge.

Muswada huo unaielezea Rwanda kuwa nchi salama na sehemu muhimu ya mipango ya serikali ya kuwapeleka baadhi ya watu wanaotafuta hifadhi nchini Uingereza.

Muswada huo umekuwa ukikosolewa vikali na vyama vya upinzani lakini baada ya mijadala kadhaa, wabunge wa Uingereza (the Lords) walitupilia mbali pingamizi dhidi ya muswada huo jana Jumatatu, jioni.

Sunak amesema safari za ndege za kuelekea Rwanda zitaanza ndani ya wiki 10 hadi 12, baada ya lengo lake la awali kushindikana ambapo safari hizo zilitarajiwa kuanza kati ya Septemba na Desemba mwaka jana.

Hata hivyo, hii haijaisha kabisa kwani safari hizo bado zinaweza kusimamishwa na mahakama au kucheleweshwa kwa ajili ya kupata ndege ambazo zitatumiwa kuwasafirisha wahamiaji hao hadi Rwanda.

Waziri wa Mambo ya Ndani, James Cleverly amesema kupitishwa kwa muswada huo ni “kuandika historia katika mpango wetu wa kuzuwia mashua (za wahamiaji kuingia Uingereza).”

Lakini Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani, Yvette Cooper ameuita mpango huo wa Rwanda “ujanja wa gharama kubwa’’.

Mipango ya serikali imekwama tangu Novemba 2023, wakati Mahakama ya Juu ya Uingereza ilipoamua kwa kauli moja kwamba mpango huo wa kuwapeleka wahamiaji wanaotafuta hifadhi Uingereza nchini Rwanda haukuwa halali.

Baada ya pingamizi nyingi, kupitishwa kwa mswada huo ni ushindi wa kisiasa kwa Rishi Sunak. Huku uchaguzi mkuu ukikaribia, Waziri Mkuu hana muda mrefu wa kuthibitisha iwapo mpango wake utafanya kazi kwa ufanisi au la.