Trump awaita wahamiaji ‘wanyama’

0
908

Donald Trump amewaita wahamiaji wanaoingia nchini Marekani bila vibali kuwa ni “wanyama” na akasisitiza kwamba “si wanadamu” wakati akitoa hotuba huko Michigan jana.

Mbali na maneno yake hayo yaliyochukuliwa kuwa udhalilishaji kwa wanadamu wenzake, mgombea huyo wa urais wa Marekani kwa chama cha Republican amesema wala hatafuni maneno kuwaita wahamiaji haramu wanyama!

“Watu wa Chama cha Demokrati wanasema, ‘Tafadhali usiwaite wanyama. Wao ni wanadamu.’ Ninasema, ‘Hapana, sio wanadamu, sio wanadamu, ni wanyama,'” amesisitiza Trump, Rais wa Marekani tangu mwaka 2017 hadi 2021 ambaye anawania tena kiti hicho.

Katika kuyapa madai yake uzito, Trump ametoa mfano wa mwanafunzi wa uuguzi mwenye umri wa miaka 22 wa Georgia anayedaiwa kuuawa na mhamiaji kutoka Venezuela kinyume cha sheria na kwamba hata kijana wa Michigan, Ruby Garcia, mwenye umri wa miaka 25 pia aliuliwa na mtu ambaye polisi wanahisi ni mhamiaji haramu.