Mbu mpya agunduliwa

0
267

Aina mpya ya mbu anayeeneza ugonjwa wa malaria kwa kipindi cha mwaka mzima imegundulika nchini Kenya.

Asili ya mbu huyo ni Asia Kusini, mbu huyo ‘Anopheles stephensi’, na anadaiwa kuwa ni sugu kwa dawa za kuua wadudu zilizopo barani Afrika.

Alitambuliwa wakati wa utafiti wa kawaida katika kaunti ya Marsabit Kaskazini mwa Kenya baada ya takwimu za hospitali za karibu kuonesha ongezeko la malaria kwenye kaunti hiyo japo haikuwa msimu wa malaria kama ilivyozoeleka.

Mbu wa aina hiyo ambao ni vamizi, wanaweza kustawi katika misimu ya kiangazi na ya mvua na wanaweza kuzaliana popote.

Watafiti wana wasiwasi kuwa maambukizi ya malaria sasa yataendelea mwaka mzima badala ya kuwa ya msimu, na hivyo kuwa vigumu kutokomeza ugonjwa wa malaria ambao ni mojawapo ya vyanzo vikuu vya vifo vya watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano.