Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi wakutana Dodoma

0
2241

Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi nchini wametakiwa kujiepusha na vitendo vya rushwa na kuwa wazalendo na wabunifu katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Rai hiyo imetolewa jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Ashatu Kijaji wakati akifungua Kongamano la Tisa la Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi nchini.

Amesema kuwa takwimu zinaonyesha kuwa kuna viashiria vya rushwa kwenye miradi ya umma, na hivyo kuwataka wataalamu wa manunuzi na ugavi kuepuka vitendo hivyo.

Dkt Kijaji amesema kuwa program na miradi mingi ya serikali haiwezi kufanyika bila kuhusisha ununuzi na ugavi na kuwataka wataalamu hao kuwa waadilifu na kufanya kazi kwa ujuzi na weledi.

Kuhusu ujenzi wa Tanzania ya viwanda, Dkt Kijaji amesema kuwa viwanda vitachochea utoaji wa ajira, ongezeko la pato la Taifa, pato la mtu mmoja mmoja na kufanya maisha ya Watanzania kuwa bora zaidi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi nchini  Dkt Hellen Bandiho amesema kuwa hadi kufikia Disemba Mosi mwaka huu, Bodi hiyo imesajili jumla ya wataalamu 10,863 katika ngazi mbalimbali za ununuzi na ugavi.

Kongamano  hilo la Tisa la Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi nchini linafanyika kwa muda wa siku tatu  na kuhudhuriwa na washiriki kutoka mikoa yote ya Tanzania.