Bei ya Mwani yaongezeka

0
633

Wakulima wa Mwani katika kijiji cha Mungoni, Zanzibar wameendelea kunufaika na zao hilo kwa kupata bei nzuri ya kati ya shilingi elfu moja mpaka shilingi elfu mbili kwa kilo moja.

Wakulima hao wameyasema hayo baada ya Rais wa Benki ya Dunia Ajay Banga kufanya ziara katika mradi wa uzalishaji Mwani unaotekelezwa katika kijiji hicho ukifadhiliwa na benki hiyo kwa mkopo wa IDA.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wanufaika wa mradi huo wamesema baada ya kupatiwa vichanja vya kuanika Mwani na boti maalumu ya kusaidia uzalishaji wameongeza uzalishaji na kupata bei nzuri ya zao hilo, hatua ambayo imewasaidia kunufaika.

Kwa upande wake Waziri wa Uchumi wa Bluu Suleiman Masoud Makame amesema, Zanzibar kwa sasa inategemea zao la Mwani kwa ajili ya mauzo ya nje huku Rais wa Benki ya Dunia akiiomba Serikali kuweka sekta ya nishati katika vipaumbele vyake ili kuwezesha upatikanji wa umeme wa uhakika utakaovutia viwanda vidogo vya kuongeza thamani ya zao hilo.

Zaidi ya Wakulima elfu 15 wamenufaika na mradi huo wa uzalishaji Mwani katika kijiji cha
Mungoni, huku
asilimia 74 wakiwa ni Wanawake.