Waziri Nape azindua kituo cha TBC Katavi

0
442

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amezindua kituo cha kurusha matangazo ya redio TBC Taifa na TBC FM kilichopo Inyonga, Mlele mkoani Katavi ambapo amesema uzinduzi huo wa kituo cha masafa ya TBC Taifa 87.9 na TBC FM 89.9 ni utekelezaji wa malengo ya serikali katika kuwafikia wananchi wote kwa lengo la kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha.

Waziri Nape amesema TBC ni chombo cha utangazaji cha umma, kimetekeleza jukumu hilo kwa vitendo kwa ushirikiano wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), na kwamba Serikali inalojukumu la kufikisha huduma ya habari, mawasiliano na teknolojia kwa wananchi wote.

Aidha, katika historia wananchi wa wilaya ya Mlele walikuwa wakipata matangazo ya redio za TBC kupitia mitambo ya masafa ya kati iliyopo Iwambi mkoani Mbeya.

“Nimefarijika sana kupata taarifa kuwa usikivu wa redio za TBC umekuwa ukiongezeka kutoka asilimia 54 (2015/16) hadi kufikia asilimia 92 baada ya kukalimika kwa miradi yote inayotekelezwa mwaka wa fedha 2022/23 nchini kote ifikapo Machi 2023,” amesema Waziri Nape.

Wakati huo huo, ametoa maagizo kwa mwakilishi wa TBC mkoani Katavi kutengeneza kipindi maalum cha kutangaza rasilimali ya asali halisi yenye ubora inayopatikana katika mkoa huo ikiwa ni ombi la Mbunge wa Katavi, Mhandisi Isack Kamwelwe alilolitoa katika hafla ya uzinduzi huo.

Waziri Nape ametoa wito kwa taasisi nyingine za umma kuhakikisha huduma nyingine zinakuwa rafiki ili miradi hii iwe na tija.

“TANESCO pelekeni huduma ya umeme, TARURA pelekeni huduma ya barabara katika maeneo ilipojengwa mitambo ya redio ambapo sehemu kubwa ni milimani, nimedokezwa bado kuna vituo vinatumia genereta,” amesema Waziri Nape.