Waziri Mkuu Majaliwa aomboleza kifo cha Kibonde

0
814

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa kifo cha Mtangazaji Mwandamizi wa kituo cha redio cha Clouds, -Ephraim Kibonde ni pengo kubwa kwa Taifa, Clouds Media Group na tasnia ya habari.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo alipokwenda kuhani msiba wa Kibonde kwa niaba ya Rais John Magufuli, nyumbani kwa wazazi wa marehemu Mbezi Beach  jijini Dar es Salaam.

“Msiba huu umetushtua sana na ni tukio ambalo hatukulitarajia,  ila ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu, hivi karibuni sote tulimshuhudia akiongoza ratiba ya kumuaga aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, -Ruge Mutahaba na alienda hadi Kagera kumzika.”

Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa marehemu Kibonde enzi za uhai wake ameshirikiana vizuri na serikali katika shughuli mbalimbali, hivyo amewaomba Watanzania kuendelea kushikamana na kuifariji familia ya Marehemu Kibonde.

Kadhalika, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wazazi, watoto wa marehemu pamoja na Watanzania wote kuendelea kuwa na subira na watulivu katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mpendwa wao.

Kibonde alifariki dunia alfajiri ya  Machi Saba mwaka huu jijini Mwanza.