WATOTO 3 WASIKIA KWA MARA YA KWANZA TANGU WAZALIWE

0
312

Watoto watatu waliozaliwa na changamoto ya kutokusikia, leo kwa mara ya kwanza wameanza kusikia sauti baada ya kufanyiwa upandikizaji wa kuwekewa vifaa vya kusaidia kusikia ikiwa ni mwezi mmoja baada ya upasuaji huo unaofanywa na madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Akizungumza wakati wa kuwasha vifaa hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Mohamed Janabi amesema upasuaji huo unawapa nafasi watoto hao kusikia kama watoto wengine na kuendelea na maisha ya kawaida.

Prof. Janabi amewahimiza wazazi wenye watoto ambao wamezaliwa na hawasikii kufika hospitalini mapema ili kufanyiwa uchunguzi na kupatiwa huduma stahiki kwani hadi kufikia miaka mitano watoto wanaweza kupata huduma hiyo na kuwapa fursa ya kuishi kama watoto wengine.

Akizungumza kabla ya kuwasha vifaa hivyo, Mtaalamu wa Mashine zinazopandikizwa kwa watoto ili kuwasaidia kusikia Fayaz Jaffer amesema vifaa hivyo vinahitaji uangalizi wa hali ya juu hivyo amewasisitiza wazazi na ndugu wa watoto hao kuwaangalia watoto hao kwa karibu zaidi ili wasiharibu vifaa hivyo.

Huduma ya upandikizaji vifaa kwa Tanzania ni TZS milioni 45 ambapo mtoto akienda nje ya nchi ni karibu TZS milioni 120. Hadi sasa Hospitali ya Taifa Muhimbili imepandikiza watoto 66 tangu kuanzishwa huduma hiyo mwaka 2017.