Ulega aagiza ziundwe kamati za usuluhishi migogoro ya wakulima na wafugaji

0
139

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amewataka viongozi wa Serikali kuanzia ngazi za vitongoji, vijiji, kata na wilaya kuhakikisha wanaunda kamati za maridhiano kwa ajili ya kusuluhisha migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo imekuwa ikijitokeza katika baadhi ya maeneo na kuleta madhara kwa jamii.

Ulega ametoa agizo hilo kwenye ziara aliyoifanya katika kijiji cha Nakiu kilichopo wilayani Kilwa, mkoani Lindi baada ya kupokea kero zilizohusu migogoro mingi iliyoanza kujitokeza katika wilaya hiyo inayowahusisha wakulima na wafugaji.

Katika mkutano huo wananchi wa kijiji hicho wamelalamikia jeshi la Polisi katika wilaya hiyo kwa kutochukua hatua za haraka pale wanapopelekewa taarifa za wafugaji wanaolisha mifugo yao katika mashamba ya wakulima.

Kufuatia malalamiko hayo yaliyotolewa na sehemu kubwa ya wakulima hao, Waziri Ulega ametoa maelekezo kwa watendaji wa Serikali kuanzia ngazi za chini kuanzisha kamati za usuluhishi ili ziwe zinashughulika na migogoro hiyo mapema kabla haijakuwa mikubwa na kuleta madhara

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Zainab Kawawa katika kuhakikisha maelekezo hayo ya Naibu Waziri yanafanyiwa kazi kwa haraka amewaagiza watendaji wake kuhakikisha kamati hizo zinaundwa ndani ya wiki moja.

Kuhusu suala la kuweka njia za mifugo, Kawawa ametoa mwezi mmoja kwa wataalam mifugo kwa kushirikiana na wafugaji na wakulima kuhakikisha njia hizo zinawekwa ili kupunguza usumbufu wa mifugo katika mashamba ya wakulima.