Nchimbi ahimiza miradi kusimamiwa vyema

0
121

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi ametaka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) pamoja na taasisi nyingine za umma zinazohusika na usimamizi wa miradi kuhakikisha wanazingatia ubora na thamani ya fedha ili miradi hiyo iweze kudumu.

Dkt. Nchimbi ametoa agizo hilo wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa wakati akikagua mradi wa Kiwanja cha Ndege cha Sumbawanga utakaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 60.

Ameitaka Tanroads mkoa wa Rukwa kumsimamia vyema mkandarasi anayetekeleza mradi huo kwa ukaribu ili umalizike ndani ya muda wa mkataba wa miezi 18.

Meneja wa Tanroads mkoa wa Rukwa, Mhandisi Mgeni Mwanga amesema mradi huo ulitakiwa kuwa umetekelezwa kwa asilimia 15 tofauti na sasa ambapo upo asilimia nane tu.

Kutokana na hilo amesema wakala umewaondoa wasimamizi wa mradi ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo.

Kwanja cha Ndege cha Sumbawanga chenye urefu wa kilomita 1.7 kinajengwa kwa kiwango cha lami ambapo kunatazamiwa kurahisisha shughuli za kiuchumi ikiwemo usafiri na usafirishaji wa mazao ya kilimo na uvuvi.