Mahitaji ya jamii kipaumbele CSR

0
184

Diwani wa Kata ya Songo Songo, Mkoani Lindi, Hassan Yusuph amesema Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imekuja na miongozo kuhusu uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR) itakayotoa namna bora ya utekelezwaji wa miradi inayoendana na mahitaji ya jamii na sio miradi inayoamuliwa na kampuni mwekezajiHassan ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wataalamu wa PURA walipofanya ziara kisiwani humo kwa lengo la kutembelea miradi ambayo inatekelezwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) na Kampuni ya PanAfrican Energy Tanzania (PAET). Ameongeza kuwa miongozo hiyo inakwenda kutatua changamoto ya misuguano iliyokuwepo baina ya wananchi na wawekezaji kwani hapo awali miradi iliyokuwa ikitekelezwa ilijikita zaidi kwenye utashi wa mwekezaji na sio mahitaji halisi ya jamii husika. Katika ziara hiyo, ujumbe wa PURA umetembelea kituo kipya cha afya cha Songo Songo, bweni na maabara ya sayansi katika Shule ya Sekondari Songo Songo ambavyo vyote vimejengwa na kampuni ya PAET ikiwa ni baadhi ya miradi ya CSR inayoitekeleza kisiwani humo.Ujumbe huo pia ulisikiliza wasilisho la miradi ya CSR inayotekelezwa na TPDC ambayo ni pamoja na kutoa huduma za maji na umeme bure kwa wananchi wa kisiwa hicho huku jitihada za kuwaletea kivuko cha uhakika wananchi hao zikiwa zinaendelea.