Serikali yashauriwa kutoruhusu safari za mabasi usiku

0
405

Serikali imeshauria kusitisha utaratibu wa mabasi kusafiri usiku kutokana na uwepo wa hatari kubwa ya kusababisha majanga kwa sababu madereva wanaoendesha magari usiku huwa hawalali mchana, badala yake huwa wanafanya kazi nyingine.

Ushauri huo umetolewa bungeni jijini Dodoma na Mbunge wa Bukoba Vijijini, Dkt. Jasson Rweikiza ambapo amesema kuwa safari za usiku ni hatari na bado hakuna na uwezo wa kudhibiti magari yanayosafiri usiku.

Amesema kuwa mwaka 1987 alikuwa akifantya kazi Serikali za Mitaa mkoani Dodoma na familia yake ilikuwa ikiishi Dar es Salaam, hivyo mara nyingi alikuwa akisafiri usiku na kwamba vitu alivyokuwa akiviona barabarani ni vibaya sana.

“Usafiri wa usiku sio mzuri. Hatujaweza kudhibiti madereva wetu kuwa na nidhamu ya kulala mchana, wasafiri usiku. Mchana wanafanya kazi nyingine za kubangaiza, usiku wanaendesha gari, ajali zilikuwa ni nyingi sana,” amesema Rweikiza

Amesema kutokana na hali hiyo, aliyekuwa Waziri Mkuu mwaka 1994, John Malecela alisitisha safari hizo, hivyo ameonesha mashaka yake kufuatia Serikali kurejesha utaratibu huo.

Mchango huo umekuja siku moja baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA) kufungia mabasi mawili ya Katarama na Ally’s Star kuanza safari saa tisa usiku kutokana na vitendo ilivyoeleza vinahatarisha maisha ya abiria na watumiaji wengine wa barabara.