Wasimamizi wa uchaguzi mdogo watakiwa kuzingatia sheria

0
2278

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imewataka wasimamizi wa uchaguzi mdogo wa ubunge na udiwani utakaofanyika Septemba 16 mwaka huu katika majimbo ya Ukonga mkoani Dar es salaam na Monduli mkoani Arusha na kwenye kata 13 za Tanzania Bara kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia matakwa ya katiba, sheria na kanuni zinazosimamia uchaguzi huo.

Mwenyekiti wa NEC Jaji Semistocles Kaijage ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo kwa wasimamizi wa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi wa kata na majimbo hayo.

Jaji Kaijage amewataka wasimamizi hao kuzingatia weledi na kuepuka kufanya kazi kwa mazoea ili wapunguze na kuondoa malalamiko yanayojitokeza wakati wa uchaguzi.

Amesema kuwa uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua na taratibu mbalimbali zinazopaswa kufuatwa na kuzingatiwa na kwamba hatua na taratibu hizo ndiyo msingi wa uchaguzi mzuri wenye ufanisi usio na malalamiko au vurugu.

Katika uchaguzi huo mdogo wa Ubunge na Udiwani utakaofanyika Septemba 16 mwaka huu mgombea Ubunge katika Jimbo la Korogwe Vijijini mkoani Tanga amepita bila kupingwa na wagombea 10 wa udiwani katika kata 10 nao wamepita bila kupingwa, hivyo jumla ya kata zilizobaki zitakazoingia kwenye uchaguzi mdogo ni 13 na majimbo mawili ambayo ni Monduli na Ukonga.