Wanaohujumu viwanda vya sukari kuchunguzwa

0
2199

Serikali imeunda kikosi maalum kitakachowachunguza watu wanaohujumu viwanda vya ndani vya sukari na kusababisha mlundikano wa sukari katika viwanda hivyo.

Kauli hiyo imetolewa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage na kuongeza kuwa sukari nyingi imekua ikiingia nchini kinyume na taratibu, na kusababisha sukari ya ndani kukosa soko.

Waziri Mwijage pia ametolea ufafanuzi sukari inayozaliwa katika kiwanda cha sukari cha Mahonda kilichopo Zanzibar kwa kusema kuwa kwa sasa kiwanda hicho kinazalisha tani Elfu Nne wakati mahitaji halisi ya wakazi wa Zanzibar ni tani Elfu 20, hivyo haiwezi kuuzwa nje ya Zanzibar.

Waziri Mwijage amelazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya baadhi ya Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kuhoji ni kwa nini sukari inayozaliwa na kiwanda hicho cha Mahonda cha Zanzibar inazuiliwa kuuzwa Tanzania Bara.