Wanafunzi Monduli watembelea TAEC

0
825

Zaidi ya Wanafunzi Hamsini wa Stashahada ya ualimu kutoka chuo cha ualimu cha Monduli kilichopo mkoani Arusha,  wamefanya ziara ya mafunzo katika ofisi za  Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) zenye Makao Makuu yake Njiro, – Arusha.

Lengo la ziara hiyo ni kujifunza dhana nzima ya matumizi salama ya mionzi na namna udhibiti unavyofanyika, hatua itakayowawezesha kuwa mabalozi wazuri katika uhamasishaji wa matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania Profesa Lazaro Busagala amewaambia Wanafunzi hao kuwa elimu waliyoipata itawawezesha kuelewa matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia na kujilinda na mionzi pindi watakapokuwa wakitekeleza majukumu yao ya kikazi hapo baadaye.

Kiongozi wa wanafunzi hao wa stashahada ya ualimu kutoka chuo cha ualimu cha Monduli, – Mwalimu  Sikana Menard amesema kuwa ziara hiyo imekua na msaada mkubwa kwa wanafunzi hao ambao ni walimu watarajiwa katika kufundisha masomo ya sayansi.

Ameongeza kuwa wamekuwa wakiwafundisha wananfunzi kwa njia ya nadharia,  hivyo hatua ya kutembelea Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania kumewasaidia kujionea teknolojia za aina mbalimbali.