Waepuka adha ya kufuata mbali huduma za uzazi

0
156

Wanawake wa Kijiji cha Kwadoe, Kata ya Mamba wilayani Lushoto mkoani Tanga wameepukana na adha ya kutembea umbali wa km 18 kufuata huduma za afya ya mama na mtoto baada ya serikali kujenga jengo la huduma hiyo katika hospitali ya wilaya kwa gharama ya shilingi milion 500.

Akitoa taarifa wakati mbio za Mwenge zilipotembelea miradi mbalimbali wilayani Lushoto ukuwemo huo, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Bumbuli, Idd Msuya amesema jengo hilo linahusisha eneo la upasuaji, wodi ya watoto pamoja na wodi ya wanawake na kwamba kwa sasa limefikia asilimia 85 ya utekelezaji wake.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wenzake, Hawa Salum amesema awali walikua wanatembea umbali mrefu kufuata huduma za afya eneo la Soni, jambo lililokua likihatarisha usalama wa maisha yao kutokana na kupita misituni na kwamba zipo taarifa za akina mama waliolazimika kujifungulia vichakani.

Kwa upande wake, kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Godfrey Mzava, mbali na kupongeza hatua iliyofikiwa, amewataka wataalamu wa manunuzi serikalini kuhakikisha wanafuata mfumo wa ununuzi wa umma wa kielektroniki ujulikanao kama NeST ili kudhibiti ununuzi wa umma unaozingatia uwazi.