Ujenzi wa Terminal III wakamilika kwa asilimia 95

0
824

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametembelea mradi wa ujenzi wa jengo la tatu la abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) na kusema ameridhishwa hatua iliyofikiwa.

Mradi wa ujenzi wa jengo hilo umefikia asilimia 95 na unatarajiwa kukamilika Mei 30, mwaka huu ambapo hadi sasa tayari maeneo mengi yamekamilika ikiwa ni pamoja na sehemu za abiria wanaowasili na kuondoka.

Kufuatia kukamilika kwa uwanja huo kwa asilimia 95, Waziri Mkuu ameitaka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) ianze kukamilisha  taratibu za kuutumia uwanja huo ili mkandarasi anapoukabidhi uanze kutumika.

Kadhalika, Waziri Mkuu ameipongeza kampuni inayojenga uwanja huo kwa kazi nzuri waliyoifanya kwa sababu jengo ni zuri na linavutia. Pia amewapongeza Watanzania wanaofanya kazi kwenye mradi huo.

Awali, akisoma taarifa ya mradi huo, Mkurugenzi wa Walaka wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale alimuelezwa Waziri Mkuu kuwa jengo hilo limekamilika kwa asilimia 95.

Mhandisi huyo alisema tayari wamefanya majaribio ya kwanza ya mifumo na vifaa mbalimbali na kwamba mkandarasi anatarajia kukabidhi mradi huo Mei 31 mwaka huu. Jengo hilo linauwezo kubeba abiria milioni sita.