Tutasimamia biashara ya mazao ya mifugo

0
81

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega amesema wizara yake imejipanga kuyasimamia vema mazao ya mifugo hususan maziwa, nyama na ngozi ili yazalishwe kwa ubora na kushamirisha biashara kwa lengo la kuyafanya mazao hayo kuwa na mchango mkubwa zaidi kwenye pato la Taifa.

Waziri Ulega ameyasema hayo wakati akizungumza na wajumbe wa Bodi ya Nyama na Bodi ya Maziwa kwenye kikao kilichofanyika jijini Dodoma ambapo alipokea taarifa za utekelezaji wa bodi hizo ambazo kwa sasa zimeunganishwa na kuundwa taasisi moja itakayosimamia mazao ya mifugo.

“Tuko katika uundaji wa taasisi nyingine ya usimamizi wa mazao kwa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, tunakwenda kuunda taasisi nzuri, makini, imara, itakayokwenda kuongeza tija na kushamirisha biashara. Wadau msiwe na wasiwasi, tunatambua juhudi kubwa mnazozifanya, tumejipanga kufanya kazi kwa pamoja kuleta maendeleo ya tasnia hizi mbili na sekta ya mifugo kwa ujumla”, amesema Ulega

Waziri Ulega amewahimiza wafugaji kuzalisha zaidi maziwa na nyama zenye ubora kwani bado mahitaji ya bidhaa hizo ni makubwa ndani na nje ya nchi.