TBC yawakumbuka wahitaji

0
181

Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) limetembelea na kutoa zawadi mbalimbali za Pasaka katika kituo cha kulea Watoto cha Jerusalem Home of God’s Love For Children, kinachomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kimara.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TBC Dkt. Ayub Rioba Chacha, Mtangazaji wa kipindi cha Watoto cha TBC Shinuna Said amesema, kwa kutambua umuhimu wa uhusiano na jamii, shirika hilo limetoa zawadi za Pasaka kwa watoto hao na kufurahi nao.

Ikiwa katika kituo hicho cha kulea watoto cha Jerusalem Home of God’s Love For Children, TBC imerusha matangazo Mbashara ya kipindi cha watoto kutoka kituoni hapo huku watoto wanaoishi kituoni hapo wakionesha umahiri wao katika kuimba, kusimulia hadithi, maigizo, na uchoraji.

Akitoa neno la shukrani Mchungaji wa Usharika wa Kimara Joseph Maseghe amesema, TBC imefanya jambo jema kwa kuwakumbuka watoto hao na kuupongeza uongozi wa shirika hilo kwa hatua ya kutembelea kituo hicho.

Kituo cha kulea watoto cha Jerusalem Home of God’s Love For Children kilichoanzishwa mwaka 2019,
kinalea watoto 35 wenye umri wa kuanzia miezi saba hadi miaka 14.