Tathmini ya TAMISEMI chanzo cha panguapangua ya viongozi

0
528

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema hivi sasa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imeanza kufanya tathmini juu ya utendaji kazi wa wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, makatibu tawala wa mikoa na wilaya pamoja na wakurugenzi wa halmashauri.

Amesema kutokana na taarifa za tathmini hiyo iliyoanza kufanywa hivi karibuni ndiyo inayosababisha kuwepo kwa mabadiliko ya uongozi yaliyofanyika kwani inasaidia kufahamu nani hafanyi vizuri na nani anafanya vizuri.

“Nataka niseme kwamba TAMISEMI sasa wameanza kufanya assessment kutathmini utendaji wa wakuu wa mikoa, wilaya, ma-RAS (makatibu wakuu wa mikoa) na wengineo. Na kutokana na taarifa zile za tathmini ndio tunapojua nani anafanya vizuri, nani hafanyi vizuri na ndio maana tumefanya mabadiliko haya (teuzi na uhamisho),” amesema Rais Samia alipozungumza Ikulu ya Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuwaapisha viongozi aliowateua hivi karibuni.