Serikali yataka kuharakishwa maboresho bandari ya Tanga

0
73

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango ameiagiza Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kuhakikisha miradi yote ya maboresho ya bandari ya Tanga inakamilika ifikapo mwezi Aprili mwaka 2023, ili ianze kufanya kazi kwa ufanisi na kuruhusu meli kubwa zaidi kuanza kutumia bandari hiyo.

Makamu wa Rais ametoa agizo hilo alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa gati mbili pamoja na uongezaji kina kutoka mita 3 hadi mita 13 unaondelea katika bandari hiyo ya Tanga.

Amesisitiza ni lazima bandari hiyo iweze kufanya kazi kwa viwango na kuvutia zaidi watumiaji wa bandari katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Dkt. Mpango pia amemuagiza Meneja wa bandari hiyo ya Tanga kushughulikia haraka malalamiko ya wafanyabiashara kuhusu utendaji wa bandari hiyo ikiwemo kuchukua muda mrefu utoaji wa mizigo inayopita katika bandari hiyo ikilinganishwa na bandari za jirani.

Amesema mapungufu hayo katika bandari ya Tanga yamesababisha wafanyabishara kutumia bandari za nchi jirani na hivyo kulikosesha Taifa mapato ambayo yangetumika kuwahudumia wananchi.

Halikadhalika Makamu wa Rais ameiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kutoa ushirikiano katika kufanikisha uchunguzi unaoendelea wa kuungua moto kwa ghala la mali za Mamlaka ya Mapato Tanzania.

Amesema unahitajika uchunguzi wa kina ili kubaini wote waliohusika katika kusababisha hasara iliyojitokeza katika ghala hilo.

Miradi ya maboresho katika bandari ya Tanga inatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 429 hadi kukamilika kwake, na inatarajiwa kuongeza ufanisi kufikia kuhudumia tani milioni 3 kwa mwaka kutoka tani laki saba na nusu za hivi sasa.