Rais Magufuli awataka viongozi kuzingatia sheria

0
3115

Rais John Magufuli amewataka viongozi wote nchini kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria pamoja na kuhakikisha wanasimamia ipasavyo matumizi ya rasilimali za umma kwa maslahi ya wananchi.

Rais Magufuli ametoa maagizo hayo katika ukumbi wa halmashauri ya Wilaya ya Chato mkoani Geita wakati akizungumza na viongozi na wafanyakazi wa wilaya hiyo.

Amesisitiza kuwa viongozi wote wajenge utaratibu wa kusoma sheria na kujiepusha kutumiwa kwa maslahi ya watu binafsi.

Rais Magufuli ametolea mfano mgogoro wa makontena yanayodaiwa kuwa na samani za shule na yanayoshikiliwa na Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) katika bandari ya Dar es salaam na kusema kuwa makontena hayo yanapaswa kulipiwa kodi kwa mujibu wa sheria.

Amesisitiza kuwa Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Philip Mpango ndiye mwenye dhamana ya kupokea misaada kwa niaba ya serikali na sio mkuu wa mkoa.

“Kwa mujibu wa sheria ya Madeni, Dhamana na Misaada Namba 30 ya mwaka 1974 (kama ilivyorekebishwa na sheria namba 9 ya mwaka 2003) kifungu cha 3, 6, 13 na 15, Waziri wa Fedha na Mipango ndiye mwenye mamlaka ya kukopa nje na ndani, kutoa dhamana na kupokea misaada kwa niaba ya Serikali.

“Kwa msingi huo, hakuna mtu yoyote mwenye mamlaka ya kukopa, kutoa dhamana na kupokea misaada kwa niaba ya serikali bila mtu huyo kukasimiwa mamlaka hayo na Waziri wa Fedha kwa mujibu wa sheria hiyo” amesisitiza Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli amewataka Madiwani wa halmashauri zote nchini kuhakikisha wanasimamia kwa ukaribu matumizi ya fedha za bajeti ikiwa ni pamoja na kuhakikisha fedha hizo zinaelekezwa katika miradi na huduma zenye kujibu kero na kuboresha maisha ya wananchi badala ya kuacha zikitumiwa kulipana posho za vikao na safari zisizo na tija.

“Nafahamu kuwa hata nyie Madiwani huwa mnakaa kikao siku moja na mnataka kulipwa posho ya siku mbili au tatu, au mtumishi wa halmashauri anasafiri kwa siku mbili lakini anaandikiwa posho za siku nne, nataka mchezo huu ukome, elekezeni fedha kwenye mahitaji muhimu ya wananchi, Wakurugenzi na Wakuu wa Wilaya simamieni hilo” amesema Rais Magufuli.

Katika mkutano huo ambapo alianza kwa kupokea maswali, kero na maoni ya wafanyakazi na viongozi, Rais Magufuli amewahakikishia kuwa serikali ya awamu ya Tano imedhamiria kujenga uchumi wa kujitegemea na kutatua kero za wananchi wakiwemo wafanyakazi wote bila kubagua na amewataka viongozi wa Wilaya ya Chato kuwa wabunifu wa namna ya kuharakisha maendeleo ya wananchi badala ya kubweteka kwa kutegemea kupendelewa naye kwa kigezo cha kuwa mwananchi wa Chato.