Rais Magufuli akutana na viongozi wa kimataifa Ikulu

0
352
Rais John Pombe Magufuli akiwa katika mazungumzo na Mwakilishi wa Jumuiya ya Ulaya (EU) hapa nchini Balozi Manfredo Fanti aliyeongozana na Balozi Emilio Rosetti alipokutana naye Ikulu jijini Dar es salaam Februari 5, 2020.

Rais John Magufuli kwa nyakati tofauti amekutana na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Dkt Stergomena Tax na Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Manfred Fanti Ikulu jijini Dar es salaam.

Baada ya mazungumzo yake na Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa SADC, Dkt Stergomena Tax amesema kuwa alikuja kutoa taarifa ya utekelezaji wa masuala mbalimbali ya Jumuiya hiyo ikiwemo uendelezaji wa viwanda na kanda huru ya biashara ambapo wamekubaliana kuendelea kuhamasisha nchi Wanachama kuendeleza viwanda ili kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
akisalimiana na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa
Afrika (SADC) Dkt. Stergomena Tax alipokutana na kufanya naye
mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaam Februari 5, 2020.

Ameelezea baadhi ya maeneo yaliyopo katika mkakati wa kukuza uchumi wa SADC kuwa ni kuendeleza miundombinu hasa ya usafiri na nishati ambayo bado ni changamoto kwa nchi za SADC, na pia ameipongeza Tanzania kwa hatua inazoendelea kuchukuliwa ikiwemo ujenzi wa barabara, reli na kuongeza uzalishaji wa umeme.

Kwa upande wake Balozi wa EU nchini Manfred Fanti amesema kuwa, mazungumzo yake na Rais Magufuli yamekuwa na manufaa makubwa ambapo wamejadili maendeleo mazuri ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na EU, na kwamba katika siku za karibuni wamekamilisha mazungumzo yaliyoruhusu kuendelea kwa mpango wa Jumuiya hiyo kuchangia bajeti ya maendeleo ya Tanzania ambapo shilingi Bilioni 132 zilizokuwa zimezuiwa zimeruhusiwa na sasa wanaandaa mpango mwingine wa miaka Saba utakaoanza mwaka huu.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
akisalimiana na Mwakilishi wa Jumuiya ya Ulaya (EU) hapa nchini Balozi
Manfredo Fanti aliyeongozana na Balozi Emilio Rosetti alipokutana naye
Ikulu jijini Dar es salaam Februari 5, 2020

Balozi Fanti amesema kuwa, kwa jinsi anavyoyaona maendeleo ya Tanzania ana matumaini makubwa kuwa EU itaendelea kufanya kazi kwa ukaribu zaidi na Tanzania.

Rais Magufuli amemshukuru Balozi Fanti kwa juhudi zake za kuimarisha uhusiano wa Tanzania na EU na amemhakikishia kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na EU katika masuala mbalimbali yenye maslahi kwa pande zote mbili.