Mhandisi aondolewe, mkandarasi asipewe kazi nyingine

0
313

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameagiza kuondolewa kwa Mhandisi Mshauri, LEA Associaties, anayesimamia ujenzi wa barabara ya Kitai – Lituhi sehemu ya Amani Makoro-Ruanda (km 35) kwa kiwango cha lami na kuutaka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuendelea kusimamia ujenzi huo.

Pia, ameagiza mkandarasi anayejenga barabara hiyo, China Railway Seventh Group, kutopewa miradi mipya mpaka hapo atakapokamilisha miradi aliyopewa katika mkoa wa Mara, Katavi ambayo nayo inaonekana kusuasua.

Bashungwa ambaye yuko Ruvuma kwa ziara ya kikazi ametoa agizo hilo leo wilayani Mbinga akikagua ujenzi wa barabara hiyo ambayo ukamilishaji wake umechelewa kwa asilimia 75 na kusisitiza hatua za kimkataba zichukuliwe dhidi ya Mhandisi Mshauri huyo.

Akitoa taarifa ya mradi, Kaimu Mkurugenzi wa Miradi kutoka TANROADS, Mhandisi Jephason Nko, amesema kuwa maendeleo ya mradi huo mpaka sasa umefikia asilimia 25 ikilinganishwa na asilimia 100 ambapo mradi huo ulitakiwa kukamilika Disemba 2023.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Labani Thomas, amesema kuwa Mchuchuma na Liganga wanaitegemea barabara hii kwani ndio barabara muhimu na ni kiunganishi cha kutoka Mkoa wa Ruvuma kupitia Nyasa kwenda mkoani Njombe kupitia Ludewa.