Dkt. Mpango awataka vijana kujiepusha na vitendo viovu

0
184

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa vijana nchini kujiepusha na matendo yote yasioendana na maadili ili waweze kuaminika katika taasisi za kifedha, katika uongozi pamoja na kuwa raia wema.

Makamu wa Rais ametoa wito huo
mkoani Dodoma wakati akifungua Kongamano la Vijana la mkoa huo.

Amesema maadili miongoni mwa vijana wengi yameporomoka ikiwemo kukosa uadilifu na hivyo kujiingiza katika vitendo visivyofaa kama vile matumizi ya dawa za kulevya, unyang’anyi, mapenzi ya jinsia moja, rushwa na utapeli.

Dkt Mpango amewasisitiza vijana kutambua kuwa uadilifu ni mtaji wa kuaminiwa na kufanikiwa, na hivyo kutoa rai kwa kongamano hilo kujadili kwa kina nafasi na wajibu wa wazazi, walezi, viongozi wa dini, kimila, vyombo vya ulinzi na usalama, vyombo vya habari na vijana wenyewe katika kujenga na kutunza maadili ya vijana wa Kitanzania.

Pia ameziagiza halmashauri nchini kuwasaidia vijana kujikwamua kiuchumi ikiwemo kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya uzalishaji mali kwa vijana ikiwemo kuanzisha kongani zinazoendana na fursa zilizopo kwenye maeneo, kuwaunganisha vijana na fursa za mitaji, kuhamasisha na kusimamia urasimishaji wa vikundi vya vijana ili viweze kutambulika.