Bunge lamkana Mbowe wabunge kuongezwa mishahara

0
797

Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekanusha madai yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe kwamba serikali imeongeza mishahara ya wabunge.

Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Kimataifa cha Ofisi ya Bunge leo Machi 23, 2024 imesema: “Tunapenda kujulisha umma kwamba madai hayo ni uzushi na upotoshaji kwa kuwa hakuna mbunge aliyeongezewa mshahara kama alivyodai.”

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, jana Ijumaa Machi 22, 2024 alipokuwa anahutubia mutano wa hadhara Mjini Babati Mkoa wa Manyara na kisha video yake kusambaa kwenye mitandao ya kijamii Mbowe alidai kwamba mishahara wabunge imeongezwa mwaka 2023 kutoka shilingi milioni 13 hadi shilingi milioni 18, jambo ambalo ofisi ya Bunge imesema si kweli.

“Hivyo, tunapenda kuwashauri na kuwasihi wananchi kupuuza madai hayo ambayo lengo lake ni kuleta taharuki pamoja na kuwagombanisha wananchi na wawakilishi wao,” imesema taarifa.

Taarifa hiyo imeongeza kwamba nyongeza ya mshahara ni suala linalozingatia bajeti na hakuna utaratibu wa aina yoyote kama huo ambao umefanyika kwa ajili ya kuwaongezea wbunge mishahara.