Wezi Nairobi watumia watoto

0
217

Wezi sugu katika mitaa mbalimbali jijini Nairobi sasa wanatumia mbinu mpya ya kuwatuma watoto kutekeleza uhalifu huo.

Msimamizi wa kituo cha polisi katika Kata ya Riruta, Sarah Kimsar amewataka wazazi kuwalinda na kuwapa ushauri watoto wao ili wasiingie katika mtego huo.

Hii ni baada ya matukio kadhaa kuripotiwa kwamba watoto wamekuwa wakitumiwa na wezi kutekeleza uhalifu.

“Tumepokea ripoti tatu kuhusu baadhi ya watoto waliotajwa kutumiwa na wezi kutekeleza wizi katika nyumba za watu. Watoto hawa wanatumika kuingia katika nyumba hizo, ambapo huiba vitu vya thamani kwa maelekezo ya wezi na kuwapelekea,” amesema Bibi Kimsar.

Ofisa huyo wa polisi amesema baadhi ya watoto wanaofikishwa kituoni hudai kuwa hawaishi na wazazi wao.

“Wengi wa watoto wakiletwa husema kuwa ni mayatima na kwamba wanaishi na walezi, wajomba au shangazi,” ameongeza Bibi Kimsar.

Bibi Carolyne Miburo, ambaye huishi eneo la Kabiria lililoko Riruta, alilkambia Taifa Jumapili kwamba alipoteza vifaa vya kielektroniki ikiwemo simu yake.

“Mwizi alikuwa ni mtoto aliyeingia katika ploti na wakazi wenzangu walimwona. Kusema ukweli baadhi ya watu walichukua hatua mikononi mwao wakamchapa na kumshurutisha atoe namba ya simu ya baba’ke. Unajua alitoa namba ya baba’ke licha ya kwamba awali kwenye kituo cha polisi alikosa kutoa akidai yeye ni yatima,” amesema Bibi Miburo.