Teknolojia mpya ya kuokoa maisha ya wahanga wa tetemeko Uturuki

0
213

Wizara ya Ulinzi ya Marekani inatumia mfumo wa teknolojia bandia kusaidia juhudi zinazoendelea za kukabiliana na maafa katika nchi za Uturuki na Syria kufuatia tetemeko la ardhi.

Tetemeko hilo la ardhi lilitotokea tarehe 6 mwezi huu na kusababisha vifo vya takribani watu elfu 46.

Mfumo huo wa teknolojia bandia xView2 bado upo katika hatua ya awali ya kuboreshwa, japokuwa kutokana na uhitaji umekwishaanza kutumika kusaidia harakati za uokozi zinazoendelea nchini Uturuki.

Mfumo huo hutumia picha za setilaiti kutambua uharibifu katika eneo lililopatwa na majanga, njia iliyoonekana kuwa ni nyepesi kulinganisha na zilizokuwa zikitumika awali.

Teknolojia ya xView2 hivi karibuni imetumika kudhibiti moto katika misitu huko Califonia na pia wakati wa juhudi za uokoaji baada ya mafuriko nchini Nepal.

Hata hivyo mfumo huo umeonekana kuwa na mapungufu kadhaa, kwani kwa sasa ili ufanye kazi unategemea picha za setilaiti zilizopigwa wakati wa mchana.

Hii inamaanisha kwa sasa hauwezi kutoa taarifa kwa haraka kwa majanga yanayotokea alfajiri au usiku, lakini pia ukusanyaji wa taarifa unahitilafiwa na kutanda kwa mawingu mengi.