Sheria mpya kuanza kutumika Morocco

0
2114

Sheria mpya ambayo inafanya vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji wa kijinsia kuwa ni uhalifu itaanza kutumika nchini Morocco hivi karibuni.

Sheria hiyo ambayo inajumuisha upigaji marufuku wa ndoa za kulazimishwa,  inafuatia kuongezeka  kwa vitendo  vya udhalilishaji dhidi ya wanawake katika miaka ya hivi karibuni.

Habari  kutoka nchini Morocco zinasema kuwa wanawake Sita kati ya Kumi wa nchi hiyo wamepitia vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji.

Chini ya sheria hiyo, watu wote watakaotiwa hatiani kwa makosa ya kudhalilisha iwe kwa kutumia maneno  ama ishara yoyote atakabiliwa na hukumu ya kifungo cha kuanzia mwezi mmoja hadi Sita jela na pia faini ya fedha taslimu.

Baadhi ya raia wa Morocco wamepongeza hatua ya kuwepo kwa sheria hiyo mpya huku wengine wakiikosoa kwa madai kuwa haitoi maana kamili ya unyanyasaji majumbani au marufuku katika vitendo vya udhalilishaji ndani ya ndoa.

Katika taarifa yake ya mwaka 2015, Shirika la Haki za Binadamu nchini Morocco lilisema kuwa zaidi ya asilimia Ishirini ya wanawake nchini humo wamekumbwa na matukio ya udhalilishaji japo mara moja katika maisha yao.