Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Zimamoto Kinondoni, Dar es Salaam, Elisa Mugisha amewataka wananchi kuwa wepesi kutoa taarifa pale panapotokea tatizo au kuwepo na taarifa za matukio yanayohitaji uokoaji.
Amesema kwa mujibu wa taarifa alizopata boti hiyo lilizama majira ya mchana na taarifa zikawafikia baadaye sana. Hata hivyo, amesema jeshi hilo kwa kushirikiana na vijana wa hapo Coco Beach maarufu kama Beach Boys wenye mafunzo maalumu ya uokoaji wamefanikiwa kuokoa watu wote waliokuwa katika boti hiyo.
Ameongeza kuwa boti hiyo iliyokuwa na watu tisa wote wameokolewa na wapo salama.
Mugisha ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na TBCDigital katika eneo maarufu la Coco Beach mkoani Dar es Salaam karibu na sehemu ajali hiyo ilipotokea.
Amesema wakati tukio hilo linatokea watu wengi waliliona.
“Ukiona tatizo lolote tupigie namba ya dharura 114 mara moja kwa simu yako hiyohiyo kwa maana watu walikuwepo wengi wanarekodi tukio (na simu zao) lakini taarifa kwetu zimechelewa kutufikia,” amesema Mugisha.