Wafundisheni Vijana Mila na Desturi za Makabila : Naibu Waziri Shonza

0
1703

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza ametoa wito kwa Wadau mbalimbali kuandaa matamasha ya kufundisha vijana maadili, mila na desturi nzuri.


Naibu Waziri Shonza ametoa wito huo wilayani Mbulu mkoani Manyara alipokuwa akifunga Tamasha la Nne la Utamaduni na Michezo la Jamii ya Wairaiq, tamasha lililolenga kupiga vita mila potofu na kuwafundisha vijana wa jamii hiyo maadili, mila na desturi za jamii hiyo ili waweze kuzitunza na kuziendeleza.


Amewataka Vijana hao wa jamii ya Wairaiq kuhakikisha wanazingatia malengo ya tamasha hilo na kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo.
“Kila jamii katika Taifa letu ikijipanga kufanya tamasha kama hili la utamaduni kwa vijana hakika tutajenga Taifa bora lenye nidhamu, uwajibikaji na wachapakazi, na hii itasadia sana kupunguza wahalifu katika jamii yetu, “amesema Naibu Waziri Shonza.
Pia ameupongeza uongozi wa Kanisa Katoliki wilaya ya Mbulu kwa kuandaa tamasha hilo lenye tija kwa vijana ambao ndiyo Taifa la kesho pamoja na Redio Habari Njema inayosimamiwa na kanisa hilo kwa kuelimisha umma kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii ikiwemo mila na desturi.
Kwa upande wake Askofu Mkuu Jimbo la Kanisa Katoliki Mbulu, – Anthony Lagweni ambaye ndiye mratibu wa tamasha hilo, ameiomba Serikali kuanzisha kituo cha kutunza kumbukumbu za kimila na kuhifadhi zana mbalimbali za jadi zikiwemo zile za muziki.


“Kuwepo kwa kituo kinachoelezea historia,utamaduni,mila na desturi za watu wa jamii ya Kiiraiq katika wilaya hii ya Mbulu kutasaidia kuongeza mapato kupitia Watalii na kutangaza asili ya jamii hii pamoja na umahiri wa watu wake katika mchezo wa riadha,’’amesema Askofu Lagweni.