Tanesco yapewa ‘Tano’ na Kamati

0
199

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imepongeza uongozi wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO), kwa jitihada zake za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini.

Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dunstan Kitandula ametoa pongezi hizo jijini Dodoma wakati Kamati hiyo ilipokuwa katika semina ya kujengewa uwezo katika masuala ya umeme, mafuta na gesi.

‘’Sisi Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini tunaipongeza Wizara ya Nishati na Shirika la umeme Tanzania kwa juhudi wanazofanya katika uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme nchini, jambo ambalo linaongeza ukuaji wa uchumi wa Taifa letu kwa kasi,” amesema Kitandula.

Akizungumza na wajumbe wa Kamati hiyo, Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato amesema kuwa lengo la semina hiyo ilikuwa ni kutoa uelewa sawa kwa wajumbe wapya na kuwaongezea uelewa wale waliokuwepo katika kamati hiyo.

Amesema semina hiyo imeandaliwa na Wizara ya Nishati kupitia TANESCO pamoja na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ili kuendelea kuwaimarisha wajumbe wa kamati hiyo kwa kuwa ndio wanaoishauri serikali katika sekta ya umeme, mafuta na gesi.