Kupanda miti ni lazima

0
155

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amesema suala la kupanda miti ni lazima na kuzitaka Halmashauri zote nchini kusimamia kwa karibu na kuhakikisha kwamba mazingira ya maeneo yao yanakuwa ya kijani, safi na ya kuvutia na zoezi hilo liwe endelevu.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akizindua kampeni ya kupanda miti, uzinduzi uliofanyika katika eneo la Mtumba jijini Dodoma.

Amesema wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini wanapaswa kutoa maelekezo kwa shule, taasisi mbalimbali na kwa wananchi ili washiriki kikamilifu katika uhifadhi na usafi wa mazingira.

Vilevile Makamu wa Rais ameziagiza Halmashauri kwa kushirikiana na TFS, kupanda aina za miti ambayo inaendana na mazingira ya maeneo waliopo pamoja na kuiwezesha jamii hususani ya vijana kupata elimu zaidi kuhusu utunzaji wa miti ili kuhakikisha wanachangia katika uhifadhi wa mazingira kwa weledi.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo amesema ajenda ya upandaji miti nchini ni maelekezo ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi inayotaja kupanda miti milioni 1.5 kwa kila halmashauri na miti milioni 40 kwa mkoa wa Dodoma pekee katika kipindi cha miaka mitano. Dkt. Jafo ameipongeza Benki ya NMB kwa jitihada wanazozifanya katika kushirikiana na serikali kwenye uhifadhi wa mazingira.