Home You and Your Family Mashindano ya paralympic yafunguliwa jijini LONDON

Mashindano ya paralympic yafunguliwa jijini LONDON

Viongozi wa Paralympic Tanzania wakiingia kwenye ufunguziMashindano ya 14 Paralympic yaliyo maalumu kwa watu wenye ulemavu yamefunguliwa rasmi hapo jana jijini London Uingerereza na Malkia Elizabeth.

Watu takribani elfu 80 waliujaza uwanja wa Olympic wa London wakishuhudia  kufunguliwa rasmi kwa mashindano hayo na huku mamilioni ya watu wengine wakifuatilia sherehe hizo za ufunguzi rasmi kupitia Luninga zao.

Malkia Elizabeth amesema ni faraja kwa mashindano hayo kurudi tena jijini London mahali ambapo yalifanyika kwa mara ya kwanza zaidi ya miaka 60 iliyopita.

Zaidi ya wanamichezo elfu 4200 kutoka nchi 164 walifanya maandamano ya kuingia uwanjani kabla ya malikia Elizabeth kutangaza rasmi kufunguliwa kwa mashindano hayo ya 14 ya paralympic.

Tanzania inawakilishwa na mwanamichezo mmoja tu katika mashindano hayo ambaye ni Zaharani Mwenemti atakayeshiriki katika mchezo wa kurusha kisahani na tufe  akiwa ameongozana na kocha wake John Ndumbaro.

Wengine walioongozana na timu ya Tanzania ni pamoja na mwenyekiti wa kamati ya michezo kwa walemavu Tanzania -paralympic , Johson  Jason pamoja na katibu wake Idd Kibwana.

Mashindano hayo ya paralympic yalianzshwa rasmi mwaka 1948 na Sir Ludwig Guttmann aliyeanzisha mashindano hayo yaliyoshirikisha wanamichezo 16 waliokuwa maveterani wa vita ya pili ya dunia na yalifanyika jijini London kwa mara ya kwanza.

Hadi sasa zaidi ya tiketi million 2.4 zimeshauzwa kwa watazamaji katika mashindano hayo yatakayofikia tamati Septmber  9 mwaka huu.

Last Updated ( Thursday, 30 August 2012 12:23 )  
Banner