Home You and Your Family Simba kuachana na wachezaji kutoka ukanda wa CECAFA.

Simba kuachana na wachezaji kutoka ukanda wa CECAFA.

Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya klabu ya Simba, Zakaria Hans Pop Uongozi wa mabingwa wa soka Tanzania bara wekundu wa msimbazi Simba umesema hautosajili tena wachezaji wa kigeni kutoka ukanda wa afrika mashariki na kati kutokana na wengi wa wachezaji hao kuwa watovu wa nidhamu na kukosa uaminifu.

Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya klabu ya Simba Zakaria Hans Pop amesema kuwa wameamua kufanya hivyo kutokana na kujifunza baada ya matukio yaliyotokea katika siku za karibuni juu ya wachezaji Nkanu Mbiyavanga aliyetimuliwa kwa utovu wa nidhamu na Mbuyi Twite aliyejiunga na mahasimu wao jadi Yanga.

Hans Pop amesema kwa sasa watakuwa wakisajili wachezaji wa kigeni kutoka ukanda wa kusini mwa afrika, afrika kaskazini na afrika magharibi pekee.

Katika hatua nyingine uongozi wa mahasimu wa jadi wa Simba katika soka la bongo klabu ya Yanga umethibitisha kuwa nyota wao Mbuyu Twite aliyesajiliwa kutoka FC Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo anatarajiwa kuwasili nchini leo mchana.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Afisa Habari wa Yanga Luis Sendeu amesema mchezaji huyo atawasili saa tisa alasiri akitokea Kigali, Rwanda.

Twite tayari ameichezea yanga mechi mbili za kirafiki dhidi ya Rayon Sports na Polisi Force za Rwanda wakati yanga ilipopata mwaliko na kucheza mechi za kirafiki nchini humo wiki iliyopita.

Yanga itacheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Coastal Union ya Tanga siku ya jumamosi kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam ambayo ni kujipima nguvu kabla ya ligi kuu soka Tanzania bara septemba mosi mwaka huu.

Last Updated ( Thursday, 30 August 2012 12:19 )  
Banner