Home You and Your Family Miss Redds Manyara apatikana

Miss Redds Manyara apatikana

Miss Redds Manyara 2012, Buya Ernest (18) akiwa na mshindi wa pili na tatu   Safari ya kumsaka mrembo wa mkoa wa Manyara-Miss Redds 2012, imehitimishwa baada ya Buya Ernest (18) kutawazwa malkia wa urembo mkoani humo baada ya kuwabwaga warembo wengine 9 walioshiriki mchuano huo katika ukumbi wa CCM mjini Babati.

Ulikuwa ni usiku uliojaa kila aina ya bashasha, nderemo na vifijo wakati warembo kumi kutoka sehemu mbalimbali za mkoa wa manyara walipojitosa kutafuta tiketi ya kuuwakilisha mkoa wa Manyara katika mchakato wa kumtafuta mlimbwende wa Tanzania.

Majaji wa shindano hilo walikuwa na wakati mgumu wa kuamua ni nani amekuwa zaidi ya wenzake kutokana na warembo wote kuonesha ushindani mkubwa, lakini bahati ikamwangukia Mbuya Ernest (18) kutoka wilaya ya Babati aliyefuatiwa na mshindi wa pili Dalina Sikawa-kutoka wilaya ya Simanjiro (20) na nafasi ya tatu ikanyakuliwa na mrembo LucyStephano (19) kutoka wilaya ya Mbulu.

Mwandaaji wa shindano hilo Aziza Rajabu Msengesi na mgeni rasmi, katibu tawala wa mkoa wa Manyara Bitegeko Claudio, wamesisitiza umuhimu wa kushiriki mashindano ya urembo mkoani humo pamoja na kutoa rai kwa wadhamini ili wajitokeze kutia joto mashindano ya urembo.

Warembo watatu walioshinda katika kinyang’anyiro hicho wamekabidhiwa zawadi mbali mbali ikiwemo kupewa nafasi ya kusoma chuo kikuu huria cha Tanzania kozi za muda mfupi Bure na mshindi wa kwanza amepewa fursa nyingine ya kusoma masomo ya mwaka mmoja chuo kimoja cha utalii kilichopo hapa mjini Babati.

Ben Mwaipaja, TBC Manyara.

Last Updated ( Monday, 04 June 2012 10:57 )  
Banner