Chimbuko la uvujaji wa mitihani nchini Tanzania lina historia ndefu inayoenda sambamba na kuundwa kwa BARAZA LA MITIHANI LA TAIFA mwaka 1974 ; mwaka mmoja baadaye mashauri kadhaa ya kuvuja kwa mitihani yalianza kuonekana.
Kila mara unapozungumza kuvuja kwa mitihani nchini lazima utaangalia kwa kina baraza hili lenye majukumu makubwa kwa mustakabali wa taifa letu katika elimu lakini kinyume chake utakuwa umechezea shere elimu yetu.
Kwa hakika, takwimu zinadhiirisha kuwa mwaka 1975 watahiniwa 72 walifutiwa matokeo yao kutokana na kugundulika kushiriki katika udanganyifu; Miaka mingine ni kama ifuatavyo: mwaka1976 (30), 1977(454),1978(22), 1979(140), na 1980(154) .
Hali hiyo iliendelea ambapo mwaka 1981(203),1982(138),1983(402), 1984(327),1985(268),na 1992 hali ilikuwa mbaya zaidi ambapo watahiniwa 1563 walifutiwa matokeo. Kama hali ilivyokuwa mwaka 2008 mitihani kadhaa ililalamikiwa kuvuja huku Baraza letu la Mitihani la Taifa likidai kuwa ni mtihani wa Hisabati(Basic Mathematics) pekee kwa kidato cha nne ndio uliokuwa umevuja. Je hiyo ni sahihi? Labda kweli! Lakini Baraza letu la Mitihani la Taifa ndilo tena linaloshugulika na mitihani ya: kidato cha sita, Stashahada ya Ualimu, Ualimu ngazi ya Cheti , N.A.B.E na Mafundi Mshundo.
Kumbukumbu zinaonyesha mwaka 1994 watahiniwa 20 wa kidato cha sita walifanya udanganyifu na matokeo yao kufutwa. Je!, hali ikoje kwa viwango vingine vya elimu? Jawabu lake ni kuwa: mwaka 1993 mtahiniwa mmoja wa stashahada ya Ualimu alifutiwa matokeo yake kwa tukio hilohilo, mwaka 1994 watahiniwa 13 walifutiwa matokeo yao kwa ngazi ya Ufundi Mshundo, mwaka 1993 watahiniwa tisa walifutiwa matokeo yao kwa kozi ya N.A.B.E.
Hatari sana kwani mwanafunzi, mwaliimu anayemfundisha na ata kiongozi anayesimami anaoinekana kushirikia katika udanganyifu na wizi wa mitihani, kweli mwana kidonda, mjukuu kovu.
Asili ya kuvuja kwa mitihani nchini Tanzania inatokana na sababu kadhaa ambazo kwa hakika zinawaingiza wadau wote wa elimu nchini petu japokuwa kumekuwepo na tabia ya kurushiana lawama kuwa upande mmoja ndio unaosababisha hilo, yaani Baraza la Mitihani. Kwanza kabisa , mara baada ya uhuru wa Tanganyika mwaka 1961 serikali huru ya Tanganyika iliweza kurithi mfumo wa elimu ya kikoloni ya kuwa na idadi ndogo sana ya wasomi kila ngazi ya elimu inapokuwa kubwa. Hii ilifanya shule nyingi kutotoa idadi ya wanafunzi kuendelea na elimu ya sekondari au wakati mwingine shule moja kupata mwanafunzi mmoja tu.
Kwa hiyo jamii nzima / wakati mwingine vijiji zaidi ya witatu hadi vitano vilikuwa vikitupia jicho nafasi moja tu, mh !Je utaipataje nafasi hiyo, aha wizi na udanganyifu ulikuwa ndio njia pekee ya kushinda shindano hilo. Pia uhaba wa shule nao ulikuwa ni kero kubwa ambapo baadhi ya mikoa ilikuwa haina ata shule moja ya sekondari na vyuo vikuu mathalani Chuo Kikuuu kimoja tu cha Dar es Salaam, hivyo ilibidi mwanafunzi kujitahidi kufaulu vizuri ili aweze kupata nafasi hiyo ya nadra/ adimu ; Penye huzia penyeza rupia, hapo ndipo hongo ya: pesa, mifugo , mazao na zawadi kadhaa walipewa walimu, wasimamizi wa mitihani wafanyakazi wa Baraza la Mitihani na viongozi wa elimu wa wilaya na mikoa ili waweze kufanikisha ufisadi huo. Nao Uhaba wa walimu wenye sifa kwani wakati wa kisomo cha Ngumbalu miaka ile 1970 na ile ya 1980 ili weza kuibua walimu wa Universal Primary Education(U.P.E) ambao walianza kazi ya kufundisha, kuokoa jahazi la uhaba wa walimu mashuleni.
Walimu hao walitumika kufundisha madarasa ambayo wengine hawakuwa na uwezo wa kufundisha na ikafanya wanafunzi wengi kushindwa kufanya vizuri kwani walimu wenye sifa walikuwa wachache sana . Ili kufaulisha basi ilibidi kufanya ujanja huo wa kuvujisha mitihani tu. Aidha, tabia ya kutojiamini miongoni mwa walimu ambayo iliwafanya wanafunzi wao kutojiamini iliibua hali ya wizi wa mitihani. Mashindano miongoni mwa shule na shule, walimu na walimu yalibua hilo pia, shule zao kufanya vizuri na kupewa vyeo na zawadi kwa walimu waliofaulisha sana liliwashawishi walimu wengine kufanya hivyo.
Sababu nyingine ni ile dhana ya kuwa wale wanafunzi waliokosa nafasi ya kuingia kidato cha kwanza na ngazi zingine za elimu kuwa wamefeli, ambayo inakwenda kinyume na elimu ya jadi katika jando na unyago ambao kila anayeshirika mwishoni uhitimu na kwa kiwangi kimoja na sawa, ilifanya wazazi wengi na wanafunzi kukataa hilo na kutumia mbinu kukwepa kufeli.
Gharama kubwa ya karo kwa shule binafsi ilifanya wazazi wengi kushindwa kusomesha watoto wao hivyo wazazi wengi kushindwa kumudu hilo, kwa hiyo mbinu nyingi zilitumika katika kupata nafasi kwenye shule za umma.
Bila shaka athari ya kuvuja mitihani ni nyingi lakini baadhi ya athari hizo: kwanza inawanyima haki wale walliofanya mtihani bila ya udanganyifu kuweza kuendelea na masomo na kumpa mtu asiye na sifa nafasi hiyo muhimu.
“Bila shaka mwezangu unayesoma Insha hiii waweza kuwa ni miongoni mwa walionufaika na njia hiyo haramu katika kupanda ngazi kielimu toka kiwango kimoja cha elimu kwenda kingine.” Najiuliza tu.
Athari nyingine ni hii, vyeti vya kitaaluma vitashindwa kutoa picha halisi ya uwezo wa mtu kitaaluma na kufanya majukumu mengi kutofanyika ipasavyo mathalani mahospitalini, kwenye ujenzi na kwenye taaluma zingine. Hilo linaweza kufanya ata taifa letu kukosa maendeleo katika nyanja kadhaa na kuendelea na kilio cha kila mara kuwa taifa letu ni masikini. Kwa upande mwingine hali hii inafanya ata kuweza kuwapoteza Watanzania wenye vipawa vya taalauma .
Je tunaweza kudhibiti hali hiyo? Jibuni ndiyo kwani, penye nia pana njia. Hali hii inaweza kudhibitiwa kwa kila Mtanzania kwa nafasi yake kufanya mambo yafuatayo: Kwanza, watunzi wa mitihani wawe watu makini , huku wakipewa posho ya kutosha wakati wa kufanya kazi hiyo, pia wakati wa utunzi wa mitihani ni vema aina za maswali ambayo yanashawishi udanganyifu kutopendwa kutumiwa au kuwa machache sana mathalani maswali ya kuchagua herufi ya A-E ambapo ishara kadhaa zimekuwa zinatumiwa na wanafunzi kupeana majibu ndani ya chumba cha mtihani.
Baraza la mitihani kutokana na kuwepo na Watanzania wengi wanaosoma linaweza kujiendesha kibiashara hivyo ni vema kuwa na ofisi za mikoa. Mitihani isiwe inakaa mashuleni kwenye ofisi za maafisa elimu au polisi na usafirishaji uwe wa tekinolojia ya sasa kwa kutumia ‘flash’ yaani ‘soft copy’ na siyo karatasi zote toka Dar es Salaam. Pia wanaweza kusafirisha nakala chache yaaani mojamoja kila somo alafu ofisi za mikoa za Baraza ziwe na mashine za kurudufu ili kufanya kazi hiyo muda mfupi kabla ya mtihani kuanza na siyo mitihani kukaa mwezi mzima ofisini kwa Mkuu wa Shule au kwa Afisa Elimu .
Watendaji wakuu wa baraza ni vema kufanya kazi hiyo kwa mkataba na isiwe ya kudumu kwani wengine inawafanya kuzoea kazi na wakati mwingine kushindwa kutekeleza majukumu yao. Somo la uaminifu katika mitihani kuanza kutolewa kwenye ngazi zote za elimu kuwekwa kwenye mihtasari yote kama vile: somo la usalama barabarani, elimu ya UKIMWI na elimu ya mazingira zinavyotolewa mashuleni na vyuoni.
Pia yule atakayehusika na uvujaji wa mitihani ni vema kupewa adhabu kubwa kwani sawa na yule aneyehujumu uchumi: mwanafunzi kama akingundulika ni vema nafasi ya kusoma na kufanya mitihani isitolewe tena. Wadau wote wa elimu hasa walimu, wanafunzi, wazazi na vyama vya wadau wote wa elimu kama vile Chama Cha Walimu (C.W.T) na taasisi binafsi kama vile Haki Elimu ni vema kunyanyua sauti zao kupinga hilo kwani kwa hakika elimu yetu inaweza kwenda pahala pabaya kutokana na kufumbia macho hali hii tete inayochipua kama uyoga.
Mitihani ya mwisho kama vile ule wa Darasa la Saba, Kidato cha Nne na Sita ni vema kuwa na sehemu ya asilimia 50 kutoka maendeleo ya nyuma: mazoezi, majaribio na mitihani ya mwanafunzi kwa madarasa ya nyuma na asilimia inayobaki kuwa ni ya mtihani wa mwisho. Isiwe kqma ilivyo sasa Baraza la Mitihani japokuwa linapelekewa alama hizo lakini zimekuwa zinabaki katika makabrasha ya baraza tu bila matumizi yoyote yale.
Hili ni tatizo na wajibu wangu mimi na wewe kuhakikisha tunalitatua, si jukumu la Haki Elimu, CWT, Wizara ya Elimu, au Bi Joyce Ndalichako pekee. Watanzania tuamke na kupinga uvujaji na wizi wa mitihani nchi petu. Kinyume chake taifa letu linaweza kupata wasomi wa ngazi ya Udakitari wa falsafa kwa wizi wa mitihani. Mimi sipendi , haki elimu hawapendi, nao CWT kwa niaba ya walimu hawapendi, vipi wewe?.
Adeladius Makwega TBC Dar es Salaam.

.jpg)
.jpg)
.jpg)
.jpg)