Waswahili wanasema uchungu wa mwana aujuaye mzazi. Asilimia kubwa ya wazazi wangependa kuona watoto wao wakiwa na maisha mazuri na kustawi hata ikibidi, wastawi kuliko wazazi wao. Hao ni wazazi wenye upendo wanaotaka watoto wao wapate elimu nzuri.
Kazi hii si rahisi kiasi hicho, wakati mwingine inahitaji kutoa jasho, hasa kwa wale wazazi wanaotoka katika familia za kipato cha chini. Nchini MEXICO hali sio tofauti sana na TANZANIA, wapo watu wanaokula kwa jasho, au walala hoi, kama huku kwetu wakitafuta riziki kwa tabu ili watoto wao wawe na maisha mazuri.
Wakulima nchini MEXICO hulazimika kwenda kulima maeneo ambayo hayana barabara na hivyo kutumia kamba kama daraja kuvuka kutoka katika mlima mmoja hadi mwingine wakiwa na mazao.
Wakulima hawa wanalima majani ya COCA ambayo hutumika kutengenezea dawa mbalimbali za maumivu, ingawa wafanyabiashara haramu wa dawa za kulevya hutumia majani haya haya kutengenezea COCAINE.
Zoezi hili ni la hatari, kwani wapo waliokufa wakiwa katika harakani za kuvuka mabonde makubwa kuelekea upande mwingine. Hii yote ni kuzitafutia familia zao riziki.
Kwa kihispania au kispanyora wanasema, EL CAMINO DE LA MWETTE, au kwa kiingereza ni THE ROAD OF DEATH, na sisi waswahili tunatafsiri njia ya mauti.
Ni barabara wanazopita wakulima hawa na mizigo mizito baada ya kuvuka kwa kamba na kuingia kwenye mabasi wakielekea katika jiji la maraha jiji la LA PAZ tayari kuuza mazao yao.
Pesa wanazopata ni kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na masomo ya watoto wao ili na wao wasifanye kazi ya kuning’inia kwenye kamba watakapokuwa wakubwa. Uchungu wa mwana.
