Mkuu wa mkoa wa Arusha Magessa Mulongo amewaomba viongozi wa dini kuiombea taifa liepukane na wenye tamaa ya madaraka ili kulinusuru taifa lisiingie kwenye machafuko bila sababu za msingi.
Mulongo ameyasema hayo katika ibada maalumu ya kusimikwa kitini kwa Askofu Hotay kuwa Askofu wa dayosisi ya Mlima Kilimanjaro kwenye kanisa la Christ Church Jijini Arusha.
Akitoa salamu za serikali katika ibada hiyo Mulongo ameelezea kusikitishwa kwake na tabia iliyoibuka miongoni mwa Watanzania kwa kila mmoja kutaka kuwa kiongozi au Rais kwa kumvunja vunja na kumkwamisha Rais aliyeoko madarakani.
Naye Mkuu wa Kanisa Anglikana nchini, Askofu Dk Valentino Mokiwa akihubiri kwenye ibada hiyo ametangaza msamaha kwa waumini watatu waliofungua kesi kumpinga Askofu Stanley Hotay kusimikwa na kuwaasa kurejesha imani yao kwa kanisa.
Kwa upande wake Askofu Stanley Hotay aliungana na kauli ya Askofu Mkuu Dk Mokiwa kwa kutangaza msamaha kwa wote waliompinga na kuwaomba waanze maisha mapya kwa kutumia akili zao kwa lengo la kutangaza utukufu na ufalme wa Mungu badala ya kulumbana kwa utumishi wa kiroho.
Ibada hiyo ya kumsimika Askofu Hotay imefanyika baada ya Mahakama kuu Kanda ya ARUSHA kutupilia mbali pingamizi ililowekwa na waumini watatu wa kanisa hilo.
Khalifa Mshana, TBC Arusha.

.jpg)
.jpg)
.jpg)
.jpg)