Home Local General Simbachawene afafanua taratibu za fidia maeneo yapitiwayo bomba la gesi Lindi, Mtwara.

Simbachawene afafanua taratibu za fidia maeneo yapitiwayo bomba la gesi Lindi, Mtwara.

Naibu waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene akizungumza na wananchi wa MtwaraHuku serikali ikiwa imetenga  zaidi ya shilingi bilioni 6 kwa ajili ya fidia kwa wananchi wanaopitiwa na mradi wa bomba la gesi mikoa ya Lindi na Mtwara, kumeibuka uvumi wa kuwepo kwa kundi la watu wanaowapotosha wenzao kuhusu taratibu za zoezi hilo.

Hali hiyo imesababisha baadhi ya wananchi kuanza kudai fidia bila kukubali kwanza  kuhakikiwa mali zao zitakazopotea kupisha ujenzi wa mradi huo.

Kufuatia mazingira hayo, naibu waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene ambaye yuko katika ziara ya mikoa hiyo miwili amelazimika kutoa ufafanuzi wa taratibu za ulipaji fidia hizo.

Kwa mujibu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini(TPDC), zoezi la uhakiki kwa ajili ya ulipaji fidia kwa walioathirika na ujenzi wa bomba la gesi, limeanza mkoani Mtwara katika vijiji vya Madimba na Mngoji huku tayari kukiwa na uvumi huo.

Sanjari na hilo, naibu waziri huyo wa Nishati na Madini amezungumzia umuhimu wa wakazi wa mikoa ya Lindi na Mtwara, kuacha kuweka vikwazo katika ujenzi wa kiwanda cha saruji kinachojengwa na kampuni ya Dangote mkoani Mtwara.

Kitakapokamilika kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 6,000 kwa siku.
Kassim Mikongollo,TBC Mtwara.

Last Updated ( Friday, 31 August 2012 10:23 )  
Banner