Home Local General Nahodha aeleza chanzo cha migogoro baina ya Jeshi na raia

Nahodha aeleza chanzo cha migogoro baina ya Jeshi na raia

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga, Taifa Shamsi Vuai Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Shamsi Vuai Nahodha ametaja mambo manne yanayopelekea kuwepo kwa migogoro ya ardhi baina ya jeshi na wananchi yakiwemo maeneo kutopimwa na kupewa hati za umiliki. 

Waziri Nahodha ametoa kauli hiyo bungeni mjini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya bajeti ya mapato na matumizi ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2012/2013. 

Katika kikao cha 24 bungeni mjini Dodoma Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imeliomba bunge kupitisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2012 /2013 yenye zaidi ya shilingi Trillion moja na Billioni 86.5. 

Akiwasilisha bajeti hiyo waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha akataja mambo manne yanayopelekea uwepo wa migogoro ya ardhi baina ya jeshi na wananchi. 

Pia akaeleza kuwa wizara inakabiliwa na tatizo la kuchelewa kupokea fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo. 

Akisoma maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge, Mambo ya nje, Ulinzi na Usalama Betty Machangu, akasema ili kudhibiti kuzagaa kwa matumizi ya silaha, makampuni ya kigeni yasiruhusiwe kuweka walinzi wao.

Msemaji mkuu kambi rasmi ya upinzi katika wizara hiyo Mchungaji Israel Natse amepongeza kurejea kwa mafunzo ya JKT lakini akataka kujua sababu zilizopelekea awali mafunzo hayo kufutwa. 

Baadhi ya wabunge ambao walichangia bajeti hiyo akiwemo mbunge wa Jimbo la Donge, Sadifa Juma Khamis ameitaka serikali kuchukua hatua stahiki dhidi ya wananchi wanaovamia maeneo ya jeshi huku Deo Sanga mbunge wa Njombe Kaskazini akilia na uchakavu wa sare za askari. 

Katika hatua nyingine mbunge wa Iramba Mashariki Mwigulu Nchemba aliomba mwongozo wa Spika kuhusu baadhi ya wabunge kumtishia maisha, Spika wa Bunge Anne Makinda akapangua hoja hiyo lakini akawasihi wabunge kuacha kutumia lugha za kihuni ndani ya bunge.

Anneth Andrew, TBC Dodoma.

Last Updated ( Wednesday, 18 July 2012 03:27 )  
Banner