Home Local General Uingereza kuisadia Tanzania kukuza Uchumi

Uingereza kuisadia Tanzania kukuza Uchumi

Rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania,Jakaya Kikwete Serikali ya Uingereza imeahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii ili kufikia malengo yake ya kukuza uchumi na kuwaletea maendeleo wananchi wake.

Ahadi hiyo imetolewa jana jioni jijini London na waziri mdogo wa Uingereza anayeshughulikia maendeleo ya Kimataifa, Stephen O’brien wakati akimkaribisha rasmi Rais Jakaya Kikwete na ujumbe wake nchini humo kwa ajili ya kushiriki mkutano wa kimataifa wa Uzazi wa Mpango unaoanza leo jijini humo.

Mazungumzo kati ya Waziri huyo na Rais Kikwete yamefanyika katika hoteli ya Chuchil Hayatt Regency Jijini London.

Katika mazungumzo yake na mgeni wake, Waziri huyo amesema serikali ya Uingereza itaendelea kuongeza misaada kwa Tanzania hususan katika mpango wake wa utafutaji wa gesi  unaoendelea hivi sasa ili Tanzania iweze kunufaika na sekta hiyo.

Waziri mdogo wa Uingereza anayeshughulikia maendeleo ya Kimataifa, Stephen O’brien Waziri O’brein ambaye amewahi kuishi nchini Tanzania, mkoani Mtwara, amesema kuwa serikali yake imeridhika na namna rais Kikwete anavyoshughulikia matatizo mbalimbali yanayoikabili nchi yake hususan kupiga vita umasikini.

Kwa upande wake Rais Kikwete ametumia fursa hiyo kuipongeza serikali ya Uingereza kwa kushirikiana na Tanzania katika nyanja mbalimbali na kuishukuru nchi hiyo kwa ahadi ya kuendelea kuisadia nchi yake ili iweze kuboresha uchumi wake na hatimaye kuinua maisha ya wananchi wake.

Katika hatua nyingine Rais Kwete leo mchana atashiriki katika mjadala wa kutafuta njia bora na kukusanya fedha kwaajili ya kusaidia shughuli za uzazi wa mpango wakati wa mkutano wa kimataifa utakaojadili suala hilo unaofanyika leo katika ukumbi wa Queen Elizabeth jijini London.

Rais Kikwete ni miongoni mwa wakuu wa nchi tatu kutoka Afrika walioalikwa kushiriki katika mkutano huo wa siku moja ulioitishwa na kudhaminiwa na Serikali ya Uingereza, Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) na Taasisi ya Bill na Belinda Gates.

Mbali na Rais kikwete, viongozi wengine wa Afrika walioalikwa kwenye mkutano huo ambao pia utahudhuriwa na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameroun ni Rais Yoweri Museveni wa Uganda na Rais Paul Kagame wa Rwanda.

Ben Mwaipaja, TBC London.

Last Updated ( Wednesday, 11 July 2012 11:37 )  
Banner